Habari. (News)

About habari(picha)  0ur guest my album. My Photos News(Habari)



 
Vitambulisho: Mpigachapa wa serikali angechapa kwa Sh95bn badala Sh222bn
Na Jayson.

WAKATI serikali ikiendelea na mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya uraia ya Sh222 bilioni, imebainika kwamba kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno na kama wangemtumia Mpigachapa wa Serikali kazi hiyo ingetumia Sh95 bilioni tu.

Habari zilizopatikana zinaeleza kwamba, ingawa mpigachapa wa serikali alishaomba zabuni hiyo kufanya kazi hiyo, lakini hajachaguliwa bila ya sababu maalumu.

Siri hiyo ilifichuka juzi wakati Kamati ya Bunge ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali (Miscellaneous Amendments) ilipotembelea ofisi ya Mpigachapa Mkuu kujionea utendaji kazi ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Benson Mpesya ambaye ni Mbunge wa Mbeya mjini kupitia CCM na kugundua kuwa ofisi hiyo ya serikali ina uwezo wa kufanya hiyo kazi kwa bei nafuu zaidi.

Mbunge wa Moshi mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Philimon Ndesamburo ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo aliiambia Mwananchi Jumapili jana kuwa serikali, itoe sababu za kuikatalia Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wake,  kuandaa vitambulisho vya uraia kwa gharama ya Sh95 bilioni badala yake kung'ang'ania zabuni itakayogharimu Sh222 bilioni.

Akifafanua hoja yake mbunge huyo, alisema akiwa kwenye ziara hiyo, alimuuliza Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo, kama Ofisi yake inao uwezo wa kuchapa vitambulisho vya taifa na aliwajibu wajumbe wa Kamati ya Bunge kwamba, ofisi yake inaweza kutengeneza vitambulisho hivyo kama itapatiwa fedha.

Mbunge huyo alimkariri Chibogoyo akisema kwamba, ofisi yake ilishaomba kazi ya kuchapa vitambulisho hivyo kwa gharama ya Sh95 bilioni miaka miwili iliyopita, lakini hadi sasa hajui kinachoendelea.

Ndesamburo alisema kauli ya Mpiga Chapa iliwashitua wajumbe wote wa kamati hiyo iliyoambatana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

"Mimi ninachotaka kujua kutoka serikalini ni kwa nini isiimarishe zaidi ofisi yake ambayo mpaka sasa inachapa siri nyingi za serikali kwa kuipatia kazi hiyo hata kama ni Sh150 bilioni kwa sasa, ili kuondokana na utata  unaoendelea?" alihoji.

Mbunge huyo alisema mpigachapa mkuu alieleza kwamba, kabla ya kuomba kazi hiyo alifanya utafiti katika nchi kadhaa ikiwamo Ujerumani na kuona wazi kwamba, kazi hiyo ingefanyika kwa kiwango cha kimataifa kwa gharama ya Sh95 bilioni.

"Serikali ingepunguza gharama na kuondoa malumbano yanayoendelea kama ingetoa kazi kwa Ofisi yake (mpiga chapa), ambayo inaongozwa na mtu ambaye alikuwa Rais wa Shirikisho la Wapigachapa wakuu duniani," alisema na kuongeza:

"Mpigachapa Mkuu anasema sehemu ya fedha hizo zitatumika kununua mtambo wa kisasa ambao baada ya kuchapa vitambulisho utabaki hapa hapa nchini."

Chibogoyo alipopigiwa simu jana ili kufafanua taarifa hizo, alikataa katakata kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba, mambo ya wabunge yanatolewa na wabunge wenyewe.

Naye Mpesya licha ya kukiri kwamba kamati yake ilitembelea ofisi hiyo ili kupata maelezo mbalimbali hususan jinsi ya kuchapa sheria, hakutaka kufafanua zaidi juu ya yaliyojitokeza.

Akizungumzia hali hiyo jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, alisema kwa sasa bado mchakato huo unaendelea, hivyo hawezi kuzungumza lolote juu ya suala hilo kwa kuwa kila mmoja ameomba tenda na serikali bado inaendelea kuzichambua.

“Kwa kuwa mchakato wenyewe bado haujaanza, siwezi kusema lolote juu ya hilo, hivyo basi nakuomba usubiri mpaka zoezi hilo litakapokamilika ndipo ujue ni nani ameshinda tenda hiyo na kuniuliza swali lako,” alisema Masha.

Aliongeza kuwa kuchelewa kwa mchakato wa kutengeneza vitambulisho vya uraia, kunatokana na kumtafuta mzabuni mwenye sifa anayeweza kusimamia kazi hiyo kwa umakini.

Kazi ya kuchapisha vitambulisho vya uraia imekuwa chanzo cha mvutano mkubwa miongoni mwa wanasiasa na baadhi ya watendaji wa serikali.

Katika mkutano wa bunge uliomalizika wiki hii mjini Dodoma, Mbunge wa Karatu, Dk Wilibrod Slaa alitaka kuwasilisha hoja binafsi akidai kuwa waziri Masha ameingilia kati mchakato wa kuchapisha vitambulisho hivyo kinyume cha taratibu.

Hata hivyo, hoja hiyo ilishindwa kujadiliwa na wabunge baada ya Spika kuizuia kwa maelezo kwamba, kufanya hivyo ni kuingilia kati mchakato mzima wa zabuni hiyo unaoendelea.

Suala la kuchapisha vitambulisho vya uraia nchini, limekuwa likiingia utata mara kwa mara kutokana na baadhi ya wakubwa kudaiwa kutaka kujinufaisha na zabuni hiyo.

Mchakato wake wa zabuni ya kuchapa vitambulisho hivyo ulianza mwaka 2004 na kwamba, umekuwa ukisuasua kutokana na kuzingirwa na mizengwe.

Mradi huo ulioanza kuzungumzwa miaka ya katikati ya 1970 na ambao utagharimu kiasi cha Sh222 bilioni, unaelezwa kwamba umo katika hatua za mwisho za kutaka kutekelezwa japo taarifa zinaonyesha kwamba, ni mpango mwingine mkubwa wa ulaji fedha za umma.

Mbali na suala la vitambulisho, Ndesamburo alisema kipindi hiki ni cha wanasiasa mafisadi kujuta kwa kuwa wataendelea kuumbuliwa.

Alisema kipindi hiki ni onyo kwa viongozi waliopo madarakani kwamba wasipotekeleza wajibu na kupenda ufisadi yatawafika makubwa wakati wowote.

Kuhusu masuala ya jimbo lake alisema wapiga kura wake wapo imara na wanampenda na kuipenda Chadema.

"Nilitaka kung'atuka, lakini wanachama wenzangu Moshi mjini wamenitaka niendelee kipindi kijacho, hivyo nitagombea ili CCM waendelee 'kusota'," alifafanua.

Date::2/14/2009
Walimu waliochapwa bakora wasema adhabu ya DC bado.
Na Jayson.

PAMOJA na Rais Jakaya Kikwete kumvua madaraka na kumtimua kazi Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Albert Mnali kwa kumuamuru askari kuwacharaza viboko walimu 32, waliopata adhabu hiyo na wadau wengine wamesema hatua hiyo haitoshi na kutaka sheria ichukue mkondo na waathirika kufidiwa.

Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti, walisema kosa la DC huyo la kushambulia na kudhuru mwili ni la jinai, hivyo linapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria, ili iwe fundisho kwa wengine.

Mwalimu Avitus Leornad wa Shule ya Msingi Katerero ambaye alichapwa viboko hivyo alisema, wanaiomba serikali kumfikisha Mnali mahakamani na kuwalipa fidia wale wote waliothirika katika shambulio hilo.

Hata hivyo, alisema yeye na wenzake wamefarijika na wanampongeza Rais Kikwete kwa uamuzi huo wa haraka, katika kushughulikia tukio hilo ambalo juzi na jana liligeuka gumzo nchini kote.

“Tunampongeza rais kwa uamuzi wa haraka angalau tumefarijika kidogo, lakini hiyo haitoshi tunaiomba serikali imfikishe mahakamani na tulipwe fidia kwa kudhalilishwa na maumivu tuliyoyapata,” alisema Leornad.

Alisema, kwa upande wao suala hilo wamelikabidhi kwa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuhakikisha kuwa wanamburuza mahakamani.

Alifafanua kuwa, tukio hilo limepokewa kwa hisia tofauti na wakazi wa wilaya hiyo, ambapo wengi wao wamemuunga mkono rais kwa uamuzi wa kumtimua kazi mkuu huyo wa wilaya, huku wachache wakionyesha kutoridhika.

Juhudi za Mwananchi Jumapili kumpata rais wa CWT hazikufanikiwa baada ya simu yake ya mkononi kutokuwa hewani.

Jijini Dar es Salaam, Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mwesige Baregu alisema, pamoja na uamuzi mzuri na wa haraka wa rais kumfukuza kazi mkuu huyo wa wilaya, bado hatua kali za kisheria zinastahili kuchukuliwa dhidi yake.

Alifafanua pia, walimu hao 32 waliocharazwa viboko kama wanafunzi, wanapaswa kulipwa fidia kutokana na udhalilishwaji na maumivu waliyoyapata baada ya kuchapwa.

“Ninavyoelewa mimi hilo ni kosa la jinai kwa kushumbulia kwa nguvu. Hivyo kumfukuza kazi sawa, lakini bado sana lazima afikishwe mahakamani na walimu waliothirika walipwe fidia,” alisema Baregu.

Alitoa mfano wa mwanamuziki mmoja wa kizazi kipya ambaye alimshambulia mtu, alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa jela mwaka mmoja baadaye alitoka kwa msamaha wa rais.

“Sasa huyu kosa lake ni tofauti na la mkuu wa wilaya, yeye alishambulia mtu mmoja lakini mkuu wa wilaya aliwashambulia wengi. Hivyo ni jinai isiyosameheka,” alisema Baregu.

Mwanafunzi wa Shahada ya Pili katika taaluma ya ualimu, Siraji Jaffar alisema, viongozi wengi wa kitaifa hawajui mipaka yao ya kazi jambo ambalo linasababisha kutokea kwa matukio kama hayo.

Alisema, ili iwe fundisho kwa wengine ni lazima walimu walioathirika waende mahakamani kushtaki na kudai fidia kwa kudhalilishwa na maumivu waliyoyapata.

“Lazima ifikie wakati viongozi wetu waheshimu mipaka yao ya kazi na majukumu na wajue ni kipi wanapaswa kufanya na kipi hawapaswi,” alisema na kuongeza:

“Kutokana na matendo kama haya wanataka kuturudisha nyuma sana ambako tulikwishahama wakati wa mkoloni na machifu, ambako ilikuwa katibu kata ana uwezo wa kumfunga mtu.”

Febuari 12 mwaka huu Mnali aliamuru askari mmoja kuwachapa viboko walimu 32 wa shule tatu za msingi zilizomo wilayani humo, kwa madai kuwa wanachelewa kazini jambo alilodai limesababisha wilaya hiyo kuwa ya mwisho kimkoa katika matokeo ya darasa la saba na siku moja baada ya hatua hiyo Kikwete akamvua madaraka na kumtimua kazi.

Shilingi bilioni 17 za EPA zatengwa kuwalipa wenyewe
 
2009-02-13 
Na Mbena George.

Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Omar Yussuf Mzee, amesema Sh. bilioni 17 zilizobaki katika marejesho ya fedha zilizoibwa na makampuni 22 kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa watakaojitokeza kuzidai hadi ifikapo Juni, mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa na Mzee alipozungumza na Nipashe juzi ikiwa ni siku chache tangu Bunge liidhinishe Sh. bilioni 53 zilizochukuliwa na serikali katika Sh. bilioni 70 za marejesho ya fedha hizo, zitumike kununulia pembejeo za kilimo, kuwakopesha wakulima na kununulia dawa za mifugo.

Muswada wa serikali wa kuomba idhini hiyo kwa Bunge, uliwasilishwa bungeni Alhamisi ya wiki iliyopita na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo.

Mzee alisema serikali imefikia uamuzi huo kwa vile fedha hizo ni za wafanyabiashara hususan makampuni ya nje, na kwamba, endapo hatajitokeza yeyote kuzidai katika kipindi hicho, watazitenga kwenye Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha wa 2009/2010, Julai, mwaka huu.

``Hizo Sh. bilioni 17 zimetengwa kuwalipa watakaojitoekeza hadi mwezi Juni. Akitokea mtu tutamlipa asipotokea tutazitenga kwenye Bajeti mwezi Julai,`` alisema Mzee.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo alisema suala la mahali na namba ya akaunti zilikohifadhiwa fedha hizo, hajui na kwamba anayejua ni waziri.

Fedha hizo ziliidhinishwa na Bunge kwa ajili ya matumizi ya serikali nje ya bajeti ya mwaka 2008/09.

ACP Zombe sasa hana pakushika
 
2009-02-13 14:58:37
Na NURU lUGALA.

Mshitakiwa wa pili katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, Christopher Bageni, ameiambia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa alishinikizwa na mshitakiwa wa kwanza kwenye kesi hiyo, Abdallah Zombe, kuandika maelezo ya uongo kwa Tume ya Rais iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mussa Kipenka kuchunguza mauaji hayo.

Bageni ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni kabla ya kukamatwa, amedai kuwa Zombe alimwamrisha kuandika maelezo hayo ili kuwaokoa askari polisi ambao walibashiri baadaye wangeweza kukabiliwa na kesi ya mauaji.

Kadhalika, Bageni alidai kuwa aliambiwa na bosi wake Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kinondoni, Edward Maro, kuwa watuhumiwa wa ujambazi walikamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Magomeni wakiwa hai, lakini baadaye alishangaa kuambiwa kuwa wameuawa wakati wakipambana na polisi.

``Zombe aliniambia kuwa Jaji Kipenka alikuwa school mate (mwanafunzi mwenzake) kule Songea Boys hivyo nikiandika maelezo hayo yeye (Zombe) atamwomba Jaji Kipenka asaidie kuwaokoa vijana na kesi ya mauaji inayoweza kuwakabili na mimi kwa sababu Zombe alikuwa bosi wangu sikuwa na namna,\" Bageni aliiambia Mahakama jana.

Awali, akihojiwa na wakili wa serikali, Angaza Mwipopo, Bageni aliyakataa maelezo aliyoandika mwenyewe kwa mkono wake kwa Tume ya Jaji Kipenka.

Katika maelezo yake kwa Tume, Bageni alidai kuwa waliouawa walikuwa majambazi waliokuwa wakipambana na polisi, lakini alipobanwa na wakili huyo alikiri kuwa alitoa maelezo hayo ya uongo kwa shinikizo la Zombe ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam (RPC).

Bageni ambaye naye jana alilia wakati akitoa utetezi wake kama ilivyokuwa kwa Zombe mapema wiki hii, alikuwa akikataa kuwa hakuandika maelezo hayo tarehe 14 inayoonekana katika barua hiyo na kwamba aliandika tarehe 16.

``Mtukufu Jaji haya maelezo nimeandika mwenyewe kwa mkono wangu ila inawezekana nikawa nimesahau kuandika tarehe sahihi, lakini ieleweke kuwa niliandika baada ya kushurutishwa na bosi wangu Zombe aliyesema anataka kusawazisha mambo,`` alimwambia Jaji Salum Massati, anayeisikiliza kesi hiyo.

Wakati Bageni akitoa ushahidi huo, Zombe alionekana akihaha na akikaa mikao ya aina mbalimali huku akiwasiliana na mawakili wake na kuwaonyesha nyaraka mbalimbali, ingawa haikufahamika mara moja alikuwa akizungumza nao kitu gani.

Zombe katika kesi hiyo anadai kuwa wafanyabiashara hao kutoka Mahenge, mkoani Morogoro waliuawa wakati wakipambana na polisi katika ukuta wa Posta, jambo linalokanushwa na baadhi ya washitakiwa wenzake.

Bageni alidai kuwa baada ya Zombe kumwamuru afanye hivyo, naye binafsi aliingiwa na huruma kuona kuwa askari wake wanaweza kukabiliwa na kesi ya mauaji hivyo aliamua kuandika kuwa waliouawa walikuwa majambazi waliokuwa wakipambana na polisi.

Bageni pia alidai kuwa baada ya tukio la mauaji ya wanaodaiwa kuwa majambazi, Zombe aliwaita wakuu wa polisi wa wilaya jijini Dar es Salaam pamoja na askari walioshiriki katika tukio hilo.

Alipoulizwa na wakili Mwipopo nini alisema Zombe kwenye kikao hicho, Bageni alidai kuwa alisikia kwa masikio yake Zombe akimwamlisha Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kinondoni, Edward Maro awapandishe vyeo askari walioshiriki katika tukio hilo.

Mahojiano kati ya Wakili wa Serikali Angaza Mwipopo na Bageni yalikuwa hivi:

Mwipopo: Unasema uliambiwa na bosi wako Maro kuwa wale wanaodaiwa majambazi wamekamatwa na wamepelekwa kituo cha Magomeni ulienda kuwahoji?
Bageni: Hapana si kwenda.

Mwipopo: Hukwenda kwa sababu hukuona umuhimu huo kweli si kweli?
Bageni: Nilikuwa na shughuli zingine.

Mwipopo: Ulisema kuwa ulishughulikia matukio ya uhalifu kule Tirdo na Kijitonyama, mbona Magomeni hukwenda au haikuwa muhimu?
Bageni: Nilikuwa nafuatilia matukio mengine ya siku hiyo.

Mwipopo: Umesema hapa kwamba bosi wako Maro baadaye alikutaarifu kuwa wale waliokamatwa wakidaiwa ni majambazi wameuawa, ulimhoji kwanini wauawe wakati walishakamatwa na kuwekwa kituo cha polisi?
Bageni: Yule Maro ni bosi wangu, siwezi kumhoji ila nilimshauri kuwa afungue jalada.

Mwipopo: Hukushangaa kusikia watu waliokuwa wakishikiliwa polisi Magomeni wameuawa?
Bageni: Nilishangaa.

Mwipopo: Baada ya taarifa hiyo ulienda katika kituo cha Magomeni kujua kulikoni watu wameuawa wakiwa mahabusu?

Bageni: Sikwenda kabisa.
Mwipopo: Bosi wako Maro alikwambia watuhumiwa wa ujambazi waliuawa wakiwa wapi?
Bageni: Hakusema.

Mwipopo: Ulimwuuliza kutaka kujua ukweli wa walikouawa wale watuhumiwa?
Bageni: Hapana.

Mwipopo: Tirdo na Kijitonyama ulienda, tukio la watu kuuawa hukuona umuhimu wa kwenda?
Bageni: Nilienda kufuatilia matukio mengine.

Mwipopo: Ulipoenda kituo cha Urafiki ukitokea Oyesterbay ulitumia muda gani?
Bageni: Kama robo saa tu.

Mwipopo: Ulitumia gari aina gani?
Bageni: Defender.

Mwipopo: Unakumbuka mlikuwa na nani katika safari hiyo?
Bageni: Koplo Jumanne, ambaye alikuwa dereva wangu.
Mwipopo: Katika kitengo chako una madereva wangapi?
Bageni: Kama wanne hivi.

Mwipopo: Nitajie majina yao.
Bageni: Frank, Benedict, Selemani na mwingine nimemsahau maana pale Kionondoni sikukaa sana.
Mwipopo: Mlipofika Urafiki mlikuta kuna upungufu wa Shilingi ngapi?

Bageni: Shilingi milioni 1.3.
Mwipopo: Ulizipokea.

Bageni: Nilikataa kuzipokea baada ya kuona ni pungufu.

Mwipopo: Ehee, tueleze baada ya kukataa kuzipokea nini kilifuata?
Bageni: Tulirudi Oyesterbay.

Mwipopo: Tukio hili tuliambiwa lilitokea Sinza Palestina eneo lile liko chini ya nani?
Bageni: Chini yangu.

Mwipopo: Wanaodaiwa kuwa majambazi baada ya kukamatwa walipelekwa wapi?

Bageni: Kituo cha polisi Magomeni, maana Urafiki ni kituo kidogo tu.

Mwipopo: Ulitueleza habari za vituo vya polisi vilivyo chini ya Kinondoni, ambavyo ni Kawe, Kijitonyama na Wazo, Je, pale Oyesterbay hakuna kituo kidogo cha polisi?

Bageni: Kipo.
Mwipopo: Taarifa za tukio la ujambazi Bidco ulizipata wapi?
Bageni: Kituoni kwangu.

Mwipopo: Ulisema siku ya tukio ulikuwa Pugu, wakati wa kurudi ulitumia usafiri gani?
Bageni: Gari yangu.

Mwipopo: Aina gani?
Bageni: Mercides Benz.
Mwipopo: Una redio Call wewe?
Bageni: Yes.

Mwipopo: Mbona wakati huo ulitafutwa na ulikuwa hupatikani?
Bageni: Kule kwangu Pugu hakuna network hivyo niliamua kuizima kabisa ili kunusuru betri isiishe bure.

Mwipopo: Ulipofungua hiyo redio call yako hukusikia tukio la Bidco?

Bageni: Hapana.
Mwipopo: Ulisema hapa kuwa bosi wako Maro, ulipomweleza kuhusu tukio la wanaodaiwa kuwa majambazi, alikueleza kuwa tayari analifahamu kweli si kweli?

Bageni: Ndiyo alinieleza kuwa alishapata taarifa hizo.

Awali akiongozwa na wakili wake, Gadianus Ishengoma, Bageni alidai kuwa vituo vya polisi vinne katika Wilaya ya Kinondoni vilikuwa chini yake.

Bageni alivitaja vituo hivyo kuwa ni, Kawe, Chuo Kikuu, Kijitonyama na Wazo Hill, vyote vya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Alidai kuwa kituo cha Chuo Kikuu kilikuwa chini ya Staf Sajenti James Masoto, (ambaye ametoroka na mmoja wa washitakiwa wa kesi hiyo).

Mshitakiwa huyo alidai kuwa Januari 14, mwaka 2006 askari Mkama Shapu wa Oysterbay Polisi alimtaarifu juu ya tukio la uporaji wa fedha za Bidco kwa kutumia silaha, ambalo lilitokea barabara ya Sam Nujoma na kwamba watu walioporwa walikuwepo kituoni hapo.

Bageni alidai kuwa alimuamuru awapeleke watu hao ofisini kwake ili awahoji kuhusu tukio hilo.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Ishengoma na Bageni:
Ishengoma: Uliwahi kusikia au unalijua tukio la Bidco?

Bageni: Ndiyo nilisikia tukio la Bidco.
Ishengoma: Je, jinsi gani ulisikia na kulishughulikia?

Bageni: Siku ya Januari 14, mwaka 2006 saa 1:30 usiku, alikuja Shapu kunijulisha kuhusu tukio hilo na walioporwa walikuwepo pale ofisini.

Ishengoma: Ikawaje?
Bageni: Yule askari aliwaita wale watu ambao nakumbuka majina ya wawili Mashaka Masini na Shomari, niliwafanyia mahojiano wakaniambia ni wafanyakazi wa Bidco, walikuwa wanatoka kwenye mauzo, lakini walipofika eneo la Konoike ya zamani saa 12:30, gari lao lilizuiliwa na gari ndogo, majambazi wanne waliteremka na kuwatishia kwa bunduki na kufanikiwa kuwapora Shilingi milioni tano.

Ishengoma: Nini kiliendelea?
Bageni: Wakati naendelea na mahojiano, bosi wangu Mrakibu Mwandamizi Edward Maro aliniita ofisini kwake nikaanza kumpa taarifa ya tukio, lakini alionyesha kulifahamu zaidi yangu, ambapo alinieleza kuwa majambazi wa hilo tukio wameshakamatwa kwa hiyo aliniamuru niende kuchukua vielelezo kituo cha polisi Urafiki ambavyo ni Shilingi milioni tano na bastola moja.

Ishengoma: Endelea kueleza ulikwenda Urafiki?
Bageni: Ndiyo nilikwenda, kwa kuwa kesho yake asubuhi (Januari 15) vilikuwa vinatakiwa mezani kwa Kamanda wa Mkoa wa Dar es Salaam (Zombe).

Ishengoma: Je, alikueleza hali ya watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ikoje?
Bageni: Hapana.

Ishengoma: Ulikwenda Urafiki?
Bageni: Ndiyo, nilikwenda saa 2:00 usiku.
Ishengoma: Ulimkuta nani?

Bageni: Niliwakuta Mrakibu Mwandamizi Isuto Mantage na Mrakibu Charles Mkumbo wakiwa nje ya ofisi.
Ishengoma: Ikawaje?

Bageni: Tuliongozana tukaingia ofisini kwa Mkuu wa Kituo, Juma Ndaki, ambapo baada ya muda kidogo aliongezeka Ahmed Makelle, lakini kabla hatujaongea chochote afande Mantege alimuamuru Makelle akafuate vielelezo avilete pale tulipo.

Ishengoma: Ikawaje?
Bageni: Makelle alileta mkoba ambao afande Mantage alifungua akatoa fedha na bastola, alihesabu jumla zilikuwa Shilingi milioni 2.7, alipotaka kunikabidhi nilihoji mbona hazijatimia kama nilivyoagizwa na bosi wangu.

Mbali na Zombe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Christopher Bageni, Ahmed Makelle, Jane Andrew na Emmanuel Mabula.

Wengine ni Koplo Michael, D 2300 Abeneth, Koplo Rajabu, Rashid Lema na Festus Chenge.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 katika msitu wa Pande uliopo huko Mbezi Louis nje ya Jiji la Dar es Salaam, walimuua Ephraim Chigumbi.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa siku na mahali pa tukio la kwanza washtakiwa walimuua Sabinus Chigumbi.

Katika shtaka la tatu na nne, siku ya tukio la kwanza na la pili, washtakiwa waliwaua Mathias Lukombe na Juma Ndugu.
Kesi hiyo inaendelea leo, ambapo upande wa utetezi utamhoji Bageni

wanafunzi wa Chuo Kikuu kuburuzwa kortini.

2008-04-16 09:22:12
Na Rainelly mwenda

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kimeamua kuwasimisha masomo na kuwafikisha mahakamani wanafunzi 15 waliobainika kuratibu na kuchochea vurugu zilizotokea chuoni hapo Februari mwaka huu.

Aidha, uchunguzi umebaini kuwapo kasi ya wanafunzi wa chuo hicho, wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, aliwaambia waandishi wa habari jana, kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa mapendekezo ya kamati iliyoundwa chini ya Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Alisema mwanafunzi mwingine, marehemu Deogratius Dominick, aliyefariki baada ya kuanguka katika bwawa la kuogolea chuoni hapo, alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliobainika kuwa `vinara` wa vurugu hizo.

Profesa Mukandala, aliwataja wanafunzi hao, ambao ni miongoni mwa 53 waliotuhumiwa kuhusika katika tukio hilo, kuwa ni Makere Gachuma, Paul Mwangata, Ernest Hilu, Elisha Mwalusaka, Florence Gasto, Daniel Mwakolo na Geofrey Mhelela.

Wengine ni Makwetta Reinard, Abdulrahman Mursaly, Daniel Mhako, David Silinde, Adas Chagulani, Deogratius Shirima, Dady Igogo, Judith Damson na marehemu Deogratius, ambaye hatashirikishwa katika kesi hiyo.

Profesa Mukandala, alisema wanafunzi hao walibainika kuhusika katika vitendo vya jinai, vilivyotokana na vurugu za Februari 17 na 22, mwaka huu, kwenye hosteli ya Mabibo na sehemu ya Mlimani.

Wakati huo huo, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya mlimani (UDSM) jana wameandamana kupinga maamuzi yaliyotolewa na Kamati maalum iliyoundwa kuchunguza vurugu hizo.

Maandamano hayo ambayo hayakuwa na kibali yalikuwa ya ndani na yalianzia Chuoni hapo sehemu ya utawala na kuwahusisha wanafunzi kutoka vitivo tofauti na kuhitimishwa kwa mkutano wa hadhara.

Akizungumza Rais wa serikali ya wanafunzi, Bw. Daud Deo alisema bunge la wanafunzi litakutana ili kujadili taarifa hizo ambazo zimetolewa na kamati.

Wadau leo kujadili rasimu ya mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Habari

2008-04-16 09:23:43
Na kagema merry

Wadau wa sekta ya habari, leo wanakutana jijini Dar es Salaam, kujadili mapendekezo ya rasimu ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari wa 2008.

Taarifa ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari (MCT), Bw. Anthony Ngaiza iliyotolewa jana ilieleza kuwa, mkutano huo wa siku moja, umeandaliwa na Umoja wa Kutetea Haki ya Kupata Habari Tanzania.

Bw. Ngaiza alisema mjadala huo unatarajiwa kufunguliwa na Jaji mstaafu, Mark Bomani ambapo Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Bw. Reginald Mengi atahutubia.

Alifafanua kuwa, wasimamizi wa vyombo vya habari, wanahabari, watetezi wa haki za binadamu, maofisa wa serikali na wawakilishi wa asasi za kiraia wanatarajiwa kushiriki.

Kwa mujibu wa Bw. Ngaiza, mapendekezo yatakayojadiliwa yanatokana na mchakato wa miezi sita ambapo wadau walizunguka nchi nzima kukusanya, kupokea na kuchambua maoni ya wananchi juu ya sheria hiyo.

Aliongeza kuwa, wadau wa habari wanapendekeza sheria hiyo ijikite katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotambua haki ya kila mwananchi kupata na kusambaza habari, kujieleza na kutoa maoni bila ya kuingiliwa.

Wadau wamependekeza kwamba sheria hiyo ilinde haki ya kuanzisha vyombo vya habari na isiingiliwe na dola.

Walipendekeza pia uwepo wa uhuru wa kitaaluma na vyombo vya habari vya umma visigombee matangazo na vyombo binafsi.

Taarifa ilisema sheria kandamizi 27 zimeainishwa na kupendekeza zifutwe au kurekebishwa, zikiwemo kashfa ya jinai, uhaini na uchochezi zifutwe.

Wadau hao wanaongozwa na MCT, Taasisi ya Uhuru wa Habari Kusini mwa Afrika Tanzania (MISA-TAN), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), MOAT, Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Shirika la Elimu ya Sheria Tanzania (TANLET), Shirika la Msaada wa Sheria (nola) na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TNGP).

wabunge kumweka kitimoto Pinda.

2008-04-16 09:30:28
Na Waandishi Wetu, Dodoma

Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, kesho anatazamiwa kuwekwa kiti moto na wabunge, kuhusu tuhuma zinazomkabili Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge za kujilimbikizia mabilioni ya fedha nje ya nchi.

Habari za uhakika kutoka kwa wabunge, zilisema hatua hiyo itafikiwa ili kujua msimamo wa serikali kuhusu kashfa hiyo.

Kwa mujibu wa habari hizo, wabunge hao watamhoji Waziri Mkuu wakati wa kipindi cha nusu saa cha maswali ya papo kwa papo kinachofanyika kila Alhamisi bungeni.

``Tuhuma dhidi ya Chenge ni nzito, hii si tu kwa sababu ya kiasi cha fedha anachomiliki bali tunataka kujua vyanzo vya Dola 1,000,000 alizoweka benki huko Uingereza na sababu ya kuzihifadhi nje ya nchi,`` alisema mbunge wa CCM kutoka Kanda ya Ziwa, anapotoka Bw. Chenge kwa niaba ya wenzake.

Alisema hatua hiyo itachukuliwa bila kujali au kulinda maslahi ya chama kwa kuwa chama hakijakosa bali waliokiaibisha ni watendaji kama waziri huyo.

Bw. Chenge aliripotiwa na gazeti la The Guardian Uingereza kuwa anamiliki akaunti yenye Dola zaidi ya 1,000,000 sawa na Sh. bilioni 1.2 zilizohifadhiwa kwenye benki iliyoko kwenye visiwa vya Jersey, Uingereza.

Taasisi ya kuchunguza uhalifu wa kimataifa ya nchi hiyo inachunguza iwapo kuna uhusiano baina ya fedha hizo na ununuzi wa rada mbovu iliyoligharimu taifa zaidi ya Sh. bilioni 70 (kwa tarakimu za sasa) iliyonunuliwa Uingereza wakati wa awamu ya Rais Benjamin Mkapa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa The Guardian, Bw. Chenge alikana kuhusishwa kwa fedha hizo na rushwa ya rada, ingawa alikiri kwamba ni zake.

Wakati hayo yakisubiriwa Waziri Chenge anatarajiwa kurejea nchini leo.

Vyanzo vya habari kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa vilisema jana kuwa wakati Rais Jakaya Kikwete na Waziri Benard Membe wakielekea Marekani, mawaziri wengine waliokuwa kwenye msafara huo, akiwemo Chenge, wanatarajiwa kuingia nchini leo kwa ndege ya Emirates.

Wakati huo huo, Mhadhiri mashuhuri Profesa Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema inashangaza waziri huyo anayetuhumiwa kuendelea kubakia kwenye msafara wa Rais.

``Alitakiwa awe amewekwa kando, angepumzishwa ama kwa hiari yake au na mwajiri wake ili uchunguzi ufanyike kwanza.``

Profesa Baregu ambaye ni mtaalamu wa masuala ya sayansi za siasa, alisema haieleweki na kwa hali yeyote isingependeza Waziri Chenge aendelee kuwa katika ziara ya Rais ughaibuni huku akikabiliwa na kashfa hiyo.

``Wananchi walitegemea baada ya kashfa hiyo kuwekwa hadharani, awekwe pembeni. Kumuacha aendelee kunawafanya washuku pengine serikali haijaona kama kuna tatizo dhidi ya mtendaji wake huyo,`` alionya Profesa Baregu.

Waziri huyo alikwenda bara Asia na akiwa China alisaini mkataba wa ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere utakaojengwa Dar es Salaam.

Waziri Chenge aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika awamu ya pili aliishauri serikali katika mikataba kadhaa ambayo imezua mijadala.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Bw. Robert Manumba, alipoulizwa iwapo kurugenzi yake imeanza kuchunguza mali za waziri huyo hapa nchini alisema hapana.

Alifafanua kuwa polisi haijaanza kumchunguza kwa vile Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa (TAKUKURU) inafanya kazi hiyo.

Alipoulizwa iwapo atakamatwa kwa mahojiano atakaporejea nchini, DCI akionekana yuko makini katika matamshi yake alisema polisi haijihusishi na suala hilo bali liko kwa TAKUKURU
.

Wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wadai fedha zao

2008-04-16 12:51:04
Na ITV Habari

Wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekusanyika maeneo ya Ikulu kuiomba serikali kuwalipa fedha wanazodai kulingana na makubaliano ya mwafaka wa mwaka 2004/05.

Wakizungumza na ITV katika maeneo ya ikulu wastaafu hao wamesema wamekusanyika katika maeneo hayo kwa lengo la kuiomba serikali kulipa kiasi cha shilingi billioni mianne hamsini kulingana na madai halali kumi na tano wanayodai.

Chenge akamatwe, achunguzwe - CUF

2008-04-15 10:41:58
Na rainelly mwenda

Chama cha Wananchi (CUF), kimeitaka Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kumfukuza kazi na kumuweka chini ya ulinzi wa polisi Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, ili kuchunguza madai ya akaunti yake kukutwa na dola za Marekani milioni moja (zaidi ya Shilingi bilioni moja).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema serikali ya Rais Kikwete isipofanya hivyo haitaeleweka kwa wengi, hususan suala la kupambana na vitendo vya ufisadi.
Alisema taasisi ya uchunguzi wa masuala ya rushwa nchini Uingereza ya Serious Fraud Office (SFO) ndiyo iliyofichua uozo huo.

Profesa Lipumba alisema, akaunti ya Bw. Chenge ilikutwa na Dola za Marekani milioni moja sawa na zaidi ya bilioni moja za Tanzania zikiwa zimehifadhiwa benki katika kisiwa cha Jersey nchini Uingereza.

Alifafanua kuwa gazeti la Guardian la Uingereza lilipomhoji Bw. Chenge kuhusika na fedha nyingi kiasi hicho hakukanusha bali alidai kuwa hakuzipata kwa njia ya rushwa.

Alisema fedha hizo alizolimbikiza benki, zinadaiwa kuwa ni mgao wa dola milioni 12 zilitolewa na Bw. Shailesh Vithlan, kwa mafisadi wa Tanzania kupitia kampuni ya BAE.

Kampuni hiyo inadaiwa kupokea kwa njia ya rushwa Dola za Marekani milioni 12 kupitia rada iliyonunuliwa na serikali ya Tanzania katika utawala wa awamu ya tatu.

Wakati wa ununuzi wa rada hiyo iliyopingwa sana na Watanzania, Bw. Chenge, alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye alikuwa na jukumu la kupitia na kuidhinisha mikataba mbalimbali inayofanywa na serikali.

Profesa Lipumba, alisema kwa kutumia mshahara na marupurupu mengine ya kawaida, Bw. Chenge, asingeweza kujilimbikizia kiasi hicho kikubwa cha fedha nje ya nchi.

Aidha, Profesa Lipumba, alidai kuwa katika sakata hilo Bw. Chenge, ameweka wakili wa kumtetea kutoka nchini Marekani ambaye kwa saa moja anamlipa Dola 200, sawa na zaidi ya Sh. 200,000.

Alifafanua kuwa kumweka wakili kutoka nchini Marekani ni gharama kubwa na kuhoji alipozipata fedha za kumlipa wakili huyo.

Profesa Lipumba, alitahadharisha kuwa endapo serikali haitamchukulia hatua yoyote Bw. Chenge, bajeti yake ya mwaka ambayo hutegemea wafadhili itayumba pamoja na kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Aliishutumu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kwa kumuachia Vithlan na kumfungulia mashtaka wakati ameshaondoka nchini.

Wakati huo huo, mwanasiasa mmoja aliyepiga simu katika ofisi za gazeti hili alikumbusha kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa bungeni siku chache baada ya kuingia ikulu ambapo alikemea tabia ya viongozi kuonekana wana mali nyingi baada ya kupata madaraka.

``Kama watanzania hawajasahau, Rais Kikwete alisema kwamba kinachowaudhi wananchi na kukosa imani na serikali yao ni kumuona kiongozi akiwa tajiri baada ya kupata madaraka ya umma... Hili la Chenge ni mfano mzuri wa viongozi hao aliowasema Rais,`` alisema mwanasiasa huyo kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Alifafanua kwamba si vibaya mtu kuwa tajiri, lakini haamini kama ofisa mwandamizi wa serikali anaweza kumiliki kiasi kikubwa cha fedha kama hicho nje ya nchi.

``Tena hiyo ni akanti moja tu na zingine zilizoko nchini hazijulikani idadi ya pesa zilizomo... Labda kama atatueleza hiyo biashara anayofanya na kumuingizia pesa nyingi kiasi hicho,`` aliongeza.

Serikali ina matumizi makubwa mno - CAG

2008-04-15 10:40:47
Na jayson mbewa

Licha ya mapato ya taifa yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongezeka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali inakabiliwa na tatizo la matumizi makubwa, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick Utouh, imesema.

Mkaguzi huyo amezidi kufahamisha katika ripoti ya serikali ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2007, iliyotolewa hivi karibuni kwamba mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2007, TRA ilikusanya Sh. bilioni 254 ikiwa ni zaidi ya malengo iliyojiwekea ya kukusanya sh. bilioni 241.

Hata hivyo, Bw. Utouh alisema mfumo wa matumizi ya mapato kwa serikali umekuwa ukiongezeka mara dufu kuliko kiasi cha kinachokusanywa.

Alibainisha kuwa matumizi makubwa yanaweza kusababishwa na ukosefu wa viwango vya magari na samani ambazo serikali inanunua pamoja na kushindwa kudhibiti matumizi ya fedha katika kukarabati magari na matumizi mabaya ya mafuta.

Alitaja eneo lingine ambalo linachangia matumizi makubwa serikalini ni maofisa wake kufanya utitiri wa semina na warsha ndani na nje ya nchi.

Aidha alisema katika ukaguzi huo, imebainika kwamba serikali ni dhaifu katika kudhibiti manunuzi ya samani kwa maofisa wake.

Alisema kwa mfano, mara nyingi samani zinazowekwa katika nyumba za serikali zimekuwa zikinunuliwa kutegemeana na matakwa ya ofisa au mtumiaji, hali inayochangiwa na kutokuwa na viwango vya pamoja ambavyo serikali imejiwekea.

Alishauri kuwa moja ya mambo yanayoweza kupunguza matumizi makubwa ya fedha ni kwa serikali kuwa na viwango vya aina ya magari na samani inayozihitaji kwa taasisi zake na kudhibiti matumizi makubwa ya mafuta.

Katika hatua nyingine, Bw. Utouh alisema misamaha ya kodi isiyo ya lazima imechangia TRA kushindwa kukusanya kodi mara dufu.

Alisema licha ya TRA kukusanya zaidi ya Sh. bilioni254 kwa mwaka 2006/07, mamlaka hiyo ingeweza kukusanya zaidi ya hapo iwapo misamaha ya kodi isiyo ya lazima isingetolewa.

Alisema katika kipindi hicho, misamaha ya kodi ya asilimia 30 ilitolewa, hali ambayo iliifanya TRA isiweze kukusanya zaidi. Kufuatia hali hiyo, Bw. Utouh aliishauri serikali kupitia upya sera yake ya kutoa misamaha ya kodi kwa lengo la kuipunguza.

``Mapendekezo makubwa katika ukusanyaji wa kodi, serikali ipitie upya sera yake ya kutoa misamaha iliipunguzwe hadi kufikia kiasi ambacho inaweza kuvumilika na itolewe kwa kuzingatia maslahi ya umma,`` alishauri

TLP chupuchupu kufutwa.

2008-04-15 10:39:25
Na Nyingi baraka.

Chama cha TLP kinachoongozwa na Bw. Augustino Mrema, kimenusurika kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufutwa, kutokana na mkanganyiko wa taarifa za utendaji wake.

TLP ni miongoni mwa vyama 17 vyenye usajili wa kudumu, vinavyopaswa kukidhi matakwa ya kisheria, kama vile kuendesha vikao kwa mujibu wa Katiba inayotambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Msajili wa Vyama vya Siasa, Bw. John Tendwa, alisema taarifa za awali zilionyesha TLP kushindwa kutekeleza kigezo cha kuitisha Mkutano Mkuu wa Uchaguzi.

Bw. Tendwa, alisema kwa mujibu wa taarifa zilizopo ofisini kwake, TLP ilipaswa kuitisha mkutano huo Januari, mwaka huu.

``Tuliwaandikia barua ya kuwakumbusha kuhusu suala hilo, na wao wakatujibu kwamba, mkutano huo unapaswa kufanyika Januari mwakani, kwa hiyo sasa tunakitambua kama chama halali cha siasa,`` alisema.

Bw. Tendwa, alivitaja vyama vingine vilivyokuwa na utata katika kuhalalisha kuwepo kisheria ni DP cha Mchungaji Christopher Mtikila na NRA.

Alisema wakati kumbukumbu zilizowasilishwa na DP zilionyesha kufanyika kwa mkutano huo Desemba, chama cha NRA kilibainika kuitisha mkutano huo kati ya Oktoba na Novemba, mwaka jana.

``Tunaendelea kuvichambua vyama vyenye usajili wa kudumu, lakini hadi sasa, hakuna chama kilichobainika kutokuwa na sifa za kuwa chama cha siasa,`` alisema.

Bw. Tendwa, alisema vyama vyenye wabunge na madiwani, vimefanikiwa kutimiza kalenda za vikao vyao, na hivyo kutokuwa na usumbufu katika uwasilishi wa kumbukumbu zake.
Alivitaja vyama hivyo kuwa ni CCM, CHADEMA, CUF, UDP na NCCR-Mageuzi.

Alisema ofisi yake inaendelea kutekeleza jukumu la kuvikumbusha vyama hivyo kuwasilisha kumbukumbu, ili viendelee kutambuliwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha, alisema ofisi yake inaendelea na zoezi la kuhakiki uhai wa vyama vya siasa katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Alitoa mfano kuwa, katika mkutano wa 11 wa Bunge unaoendelea, baadhi ya maofisa kutoka ofisini kwake, wanashiriki ambapo pia wanapata fursa ya kufanya shughuli nyingine, kama vile uhakiki wa vyama kwenye mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro.

Bw. Tendwa, alisema ofisi yake imefanikiwa kuajiri wanataaluma katika fani za sheria, uchumi na sayansi ya siasa ili kuboresha majukumu yake.

``Ofisi sasa hivi huwezi kukuta watu wanapiga zogo, hapa ni kuchapa kazi tu, wanasheria wamebanwa, wachumi wamebanwa, wanasayansi ya siasa halikadhalika wamebanwa na majukumu,`` alisema.

HATUOGOPI KUFA

Na R.Mwendakaya

kutoka Darleo 30-MAY-2008. 

 Muungano wa vyama vya kambi ya siasa Nchini Tanzania vimeiomba serikali kutoa usia uliotolewa na Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Mapema iwezekanavyo. Wamesema usia huo usipowekwa hadharani wenyewe ndio wataanika hadharani endapo wakipata.Tundu Lisu kutoka chadema alisema kuwa endapo anapanda vyombo kama ndege na gari vikiwa vya hatari zaidi kamwe hawezi kuogopa kufa kwa mambo ya ufisadi wengine waliounga mkono ni pamoja na Dr.WIlbroad Slaa Mbunge wa karatu na Augustine Lyatonga mrema wa chama cha TLP.

 Jitihada za kujengwa kwa taifa la Tanzania ni kutokana na viongozi walioko madarakani pia zimechangiwa mno na vyama vya upinzani kwa kutoa habari kama za ufisadi ambazo zilionekana kudidimiza maisha ya mtanzania mwenye kipato kidogo kwa manufaa ya watu wachache.